Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Mhandisi Dkt. Richard Masika ameishukuru Serikali chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo amesema kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Taasisi hiyo imepata fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza leo Disemba 06, 2024 jijini Dar es Salaam katika mahafali ya 18 ya Taasisi hiyo Dkt. Masika amesema Taasisi hiyo inajivunia mafanikio makubwa kupitia utekelezaji wa Mradi wa Kujenga Ujuzi na Ushirikiano Afrika Mashariki (EASTRIP) ambao unawezesha ujenzi wa miundombinu ikiwemo Kituo cha Kikanda cha Umahiri wa TEHAMA (RAFIC) katika Kampasi Kuu ya Dar es Salaam pamoja na ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike.
‘’Wizara pia imetupatia mkopo wa riba nafuu kutoka serikali ya Italia ambapo sehemu ya fedha hizo inalenga kuanzisha kituo cha ujasiriamali, ubunifu, uhaulishaji wa teknolojia, hatua hii inatuwezesha kuendelea kuunda, kuendeleza na kulea teknolojia mbalimbali’’ alieeleza Dkt. Masika