Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema kuwa Masomo ya Maendeleo (Development Studies) yanapaswa kusaidia nchi zinazoendelea kufahamu mahitaji ya watu wao, kubaini mizizi ya changamoto na kuleta suluhisho jumuishi na endelevu



Hayo yamesemwa na Prof Daniel Mushi kwa niaba ya Waziri huyo Disemba 10 2024, Mkoani Morogoro wakati wa kufungua Mkutano wa Kimataifa wa Tatu wa Masomo ya Maendeleo ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe,



Prof Mushi amesema Maendeleo na Masomo ya Maendeleo ni nyanja zinazohusiana moja kwa moja na mabadiliko ya kimfumo yanayolenga ustawi wa binadamu



"Masomo ya Maendeleo yanahitajika zaidi sasa kutokana na changamoto zinazoikumba jamii za kisasa, na hivyo yanapaswa kutoa suluhisho za kitaalamu na zenye ushahidi"



kuna haja ya kuwa na mbinu za maendeleo zinazojikita katika mahitaji ya binadamu, zinazojumuisha vipengele vyote vya maisha, na zinazozingatia ushahidi wa kitaalamu huku zikilenga suluhisho yanayofaa kwa mazingira ya ndani na muktadha wa dunia. Alisema Prof Mushi



Sambamba na hilo amebainisha kuwa Masomo ya Maendeleo yameundwa mahsusi kama kozi inayogusa taaluma zote katika elimu ya juu ili kuhakikisha kuwa kila mhitimu anaelewa jinsi taaluma yake inavyoweza kuchangia maendeleo ya taifa.



Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha Mzumbe Prof William Mwegoha amesema Mkutano huu utatoa mwanga juu ya jinsi juhudi za pamoja zinavyoweza kusaidia kuleta mustakabali bora kwa kila mtu, na kuimarisha matumaini ya maendeleo endelevu katika jamii.