Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, ametoa wito kwa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) kuendelea kutumia uzoefu wake katika elimu nyumbufu kuzalisha wataalamu wengi wasio na mipaka wanaoweza kuajirika ndani na nje ya nchi ili kuleta matokeo chanya kwa taifa.
Akizungumza Desemba 5, 2024, mkoani Kigoma, wakati wa Kongamano la 34 la Wanazuoni wa OUT, Prof. Nombo amesema kuwa Wizara inajivunia uwepo wa OUT kwa kuwa kinasogeza huduma ya elimu ya juu kupitia elimu nyumbufu katika mikoa yote ya Tanzania na nje ya nchi, na kukidhi maelekezo ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, inayoelekeza kuwepo kwa elimu nyumbufu nchini.
"Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inategemea sana uzoefu wa OUT katika kuishauri wizara ili kufanikisha kuifanya elimu kuwa nyumbufu nchini," amesema Prof. Nombo.
Amesisitiza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaendelea kushirikiana kwa karibu na OUT, ikiwemo kuzalisha miradi mbalimbali inayopeleka maendeleo kwa wananchi moja kwa moja, kama utekelezaji wa miradi ya kimkakati, mfano wa Mradi wa HEET. Mradi huu licha ya kuimarisha taaluma, miundombinu na teknolojia katika taasisi za elimu ya juu, pia umetoa ufadhili kwa wasichana elfu moja walioshindwa kujiunga na elimu ya juu moja kwa moja.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mh. Thobias Andengenye, amekipongeza Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwa kutoa huduma kwa weledi mkubwa kwa kipindi chote cha miaka thelathini, hivyo kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua na kuboresha wataalamu mbalimbali nchini ambao wanashiriki ipasavyo katika kuinua uchumi wa taifa na wa wananchi mmoja mmoja.
“Ndani ya miaka thelathini, chuo hiki kimefanya mengi. Kimewapa ufadhili na masomo walimu na maafisa watendaji kata, lengo likiwa ni kukipeleka chuo kwa wananchi wa ngazi za chini kabisa lakini pia kuboresha utendaji wa kada hizo, hivyo kuunga mkono juhudi za serikali katika kupeleka huduma bora na kuimarisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi,” amesema Mh. Andengenye.
Aidha, amekipongeza chuo hiki kwa kudumisha mahusiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana utaalamu, kufanya tafiti, pamoja na kuendesha miradi mbalimbali ya pamoja kwa lengo la kuimarisha utoaji wa taaluma kwa wanafunzi wa chuo nchini.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Joseph Kuzilwa, ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa taasisi za elimu ya juu nchini, hususan kwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, katika kipindi chote cha miaka thelathini ya utoaji wa huduma za chuo hiki, ambapo ushirikiano huo umepelekea upatikanaji wa elimu bora nchini.
Aidha, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, amesema chuo hiki kimekuwa fursa kubwa kwa Watanzania, kwani kimeweza kuwapa nafasi ya kusoma elimu ya juu wale ambao wasingeweza kuipata katika mifumo ya kawaida. Elimu hii inaanza kumjenga mwanafunzi kuanzia kozi za awali hadi ngazi za umahiri. Hadi sasa, takribani wahitimu 60,000 wamepata elimu yao kupitia chuo hiki.
Kongamano la 34 la Wanazuoni wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania lilifuatiwa na mahafali ya 43 ya chuo hicho yaliyofanyika Desemba 5, 2024, katika viwanja vya Kawawa, ambapo wahitimu 4,307 walihitimu. Aidha, kongamano hili lilitanguliwa na zoezi la upandaji miti, ambapo viongozi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mkoa wa Kigoma, na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania walishiriki kupanda miche ya michikichi katika eneo la chuo hicho mkoani Kigoma.