Timu ya Benki ya Dunia Oktoba 28, 2024 imeendelea na ziara yake ya kukagua Miradi inayotekelezwa na Taasisi za Elimu ya Juu kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Maendeleo ya Kiuchumi (HEET) unaofadhiliwa na benki hiyo.



Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo katika Kampasi ya Buyu, Mratibu Msaidizi Dkt. Libereta Haule amesema kuwa mradi umewezesha kuongeza udahili wa wanafunzi katika kampasi hiyo ya awali kutoka 139 hadi kufikia 278.



Dkt. Haule ameongeza kuwa Mradi huo unahusisha ujenzi ambapo katika kampasi kutakuwa vyumba vya Mihadhara vitakavyokua na uwezo wa kuchukua wanafunzi 216, Maabara wanafunzi 125, chumba cha mkutano chenye uwezo wa kuchukua watu 150 na bweni la kuchukua wanafunzi 40.



Kaimu Mkurugenzi wa Sayansi ya Bahari Dkt. Daudi Msagameno amesema kuwa kukamilika kwa Mradi huo kutaiwezesha Taasisi hiyo kuanzisha Diploma ya Marine and Coastal Ecotourism, Shahada ya kwanza ya Uchumi wa Buluu na kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Uchumi wa Buluu.



Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia Prof. Roberta Malee amesema kuwa wameridhishwa na utekelzaji wa Mradi katika Taasisi hiyo ambapo inaonyesha utekelezaji uko mbele ya muda.


.
Naye Mkadiriaji Majengo (QS) wa Mradi Faraja amesema mradi huo ni wa miezi 18 na kwamba tayari maboma ya majengo yote yamesimama na kwamba kwa ujumla kazi imefikia asilimia 40.



Mradi wa ujenzi katika Taasisi ya Sayansi za Bahari ambayo ni moja ya Kampasi za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambazo zimepata fedha za Mradi wa HEET kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ujifunzaji na kufundishia, kujenga uhusiano baina ya mahitaji ya soko la ajira na programu za mafunzo na kuboresha usimamizi wa mfumo wa elimu ya juu nchini.