Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Afrika Kusini zimedhamiria kuimarisha mashirikiano katika nyanja ya teknolojia ya anga ili kukuza maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia na ubunifu ili kuchagiza maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi hizo mbili.



Akizungumza Oktoba 31, 2024 jijini Dar es salaam Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Afrika Kusini Mhe. Dkt. Bonginkosi Nzimande amesema nchi hiyo ipo tayari kushiriki kikamilifu ukizingatia uwepo wa Shirika la Anga la Afrika Kusini (SANSA), ambapo umesaidia kupiga hatua kubwa katika teknolojia ya anga, hivyo itatoa fursa kwa wataalam wa Tanzania kujifunza kupitia mafunzo na miradi mbalimbali ya pamoja.



Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Prof. Ladislaus Mnyone amesema kuwa hatua ya mashirikiano hayo inalenga kuongeza hamasa ya matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kuanzia ngazi za Serikali za Mitaa.



Nae Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam DIT) Mhandisi Dkt. Richard Masika amesema ushirikiano huo unahusisha ufadhili wa masomo, kubadilishana ujuzi na utaalam, hususan katika masuala ya utafiti wa anga, usimamizi wa data za satelaiti na mifumo.