Mkaguzi wa Ndani Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekonolojia Bi. Anna Mhere leo Novemba, 2024 amewatembelea washiriki wa mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule yanayowahusisha Walimu Wakuu katika kituo cha mafunzo cha Kashato-TRC kilichopo Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.



Mhere amewaeleza kuwa, walimu wana mchango mkubwa, ndio maana Serikali inaendelea kutoa vipaumbele vya mafunzo kwa walimu ili taifa liweze kupata rasilimali yenye maarifa na ujuzi stahiki kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali.



Aidha amewataka Walimu hao kutekeleza kwa vitendo mafunzo waliyopata kuleta mabadiliko chanya katika shule wanazosimamia.



"Ninawasihi walimu wote muendelee kutekeleza majukumu yenu kwa weledi, pamoja na kuimarisha maadili mema kwa watoto mnao wasimamia" alisisitiza Mhere.



Mwalimu Mkuu Shule Msingi Nyerere katika Manispaa ya Mpanda Mwl. Zuhura Kapama amesema mafunzo hayo yamewapatia uzoefu mkubwa na maarifa na kwamba yatawasaidia kuleta mabadiliko makubwa katika usimamizi na uongozi wa shule.



Mafunzo kwa Walimu Wakuu 282 kutoka katika Shule zote za msingi za mkoa wa Katavi yaliyoanza Novemba 04 hadi 06, 2024 yanatarajiwa kuhitimisha leo.



Mafunzo hayo yameendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) chini ya Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST).