Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 kuhusu elimu ya lazima kuwa ya miaka 10 utaanza Mwaka 2027/28 ambapo wahitimu wa elimu ya msingi ya miaka 6 watakutana na wahitimu wa mwisho wa elimu ya msingi ya miaka saba wote wataanza kidato cha kwanza.
Prof. Mkenda amesema hayo Mkoani Ruvuma Septemba 26, 2024 akitoa mada juu ja mageuzi ya Elimu katika Kongamano la Mafunzo kwa Umoja wa Wanawake Tanzania, ambapo ameongeza kuwa ifikapo Mwaka 2027/28 Mtoto ambaye hatakaa shuleni kwa miaka 10 hatua zitachukuliwa kwa mzazi au mlezi.
Waziri huyo amesema kuwa Wizara ilifikia hatua ya kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na kuboresha Mitaala baada ya watanzania kulalamika juu ya elimu inayotolewa na namna inavyomuandaa mwanafunzi kuingia kwenye ulimwengu wa ajira na ndipo Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maelekezo ya kufanya mapitio hayo