Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali inajenga Shule 100 za Mafunzo ya Amali Uhandisi, ili kuwawezesha Vijana kupata ujuzi na kuwa mahiri.
Prof. Mkenda amesema hayo Oktoba 01, 2024 Mkoani Tanga wakati wa uzinduzi wa Shule ya Sekondari ya Miles & Kimberly White, ambapo amesema Wizara inaendelea kusimamia mageuzi ya Elimu, ikiwemo kuweka msukumo wa mafunzo ya amali yanayojikita kwenye ujuzi zaidi.
"Mafunzo haya ni pamoja na michezo, mapishi, utalii, Kilimo, uvuvi, ufundi Umeme, Uashi na Useremala" alisema Waziri Mkenda.
Amesema kuwa Wanafunzi watakaomaliza Sekondari mafunzo ya Amali watapata cheti za Kidato cha Nne na cheti cha VETA, na wanaweza kwenda kufanya kazi za ufundi sehemu yoyote.
Aidha Prof. Mkenda ameongeza kuwa katika kuendelea kutoa za fursa za mafunzo ya ujuzi Serikali imekamilisha ujenzi Chuo cha Ufundi Dodoma na kwamba itajenga Vyuo vingine Vinne vitakavyotoa mafunzo ya ufundi Zanzibar pamoja na katika mikoa ya Mwanza, Mtwara na Kigoma.
Amepongeza hatua ya Shule hiyo Mpya kuitikia Wito wa kuifanya kuwa Shule ya Sekondari ya Mkondo Amali ambapo shule hiyo imejikita katika amali ya kilimo.