Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Charles Mahera Wilson amewataka watekelezaji wa Programu ya Kuboresha Kada ya Ualimu (GPE- TSP) kusimamia ukamilishaji wa miradi kwa wakati.



Dkt. Charles Mahera Wilson ametoa rai hiyo Septemba 27, 2024 mkoani Morogoro wakati akifunga kikao kazi cha kutathmini hali ya utekekezaji wa Program hiyo kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo amewasisitiza Watendaji hao kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati pamoja na kuishirikisha jamii ili kuleta tija ya miradi.



“Hakikisheni miradi inakamilika kwa wakati na kwa ushirikiano mkubwa na jamii inayozunguka ili iweze kuwa na tija na viwango hitajika na kuwasilisha taarifa zilizo sahihi kila robo mwaka kulingana na matakwa ya Mfadhili wa Programu” alisema Dkt. Mahera.



Dkt. Mahera pia amewataka kufuatilia ahadi zilizowekwa na Wadau wa ndani pamoja na kuweka Mpango wa Mafunzo ya Walimu Kazini (MEWAKA) kwenye mfumo wa kazi zinazotekelezwa (PEPMIS) kwa viongozi wa ngazi ya Mkoa, Halmashauri, Kata na Shule ili kiwe kigezo cha kipaumbele kwenye upimaji wa utendaji kazi kuwezesha kupata takwimu sahihi za walimu wanaoshiriki kwenye mafunzo kwa ngazi husika.



Mwenyekiti wa kikao kazi hicho ambaye ni Mratibu wa GPE Mkoa wa Njombe Mwalimu Leonard Msendo ameahidi kutoa taarifa za utekelezaji wa ahadi za wadau kama Wafadhili wenza kwenye kipengele cha (Multiplier Grants) ili kuweza kupata kiasi cha Dola za Kimarekani 84.6 sawa na Shilingi Bilioni 212.3 kilichotengwa na Wafadhili kwa Tanzania pamoja na kuandaa taarifa za utekelezaji wa program hiyo.



Tanzania ni mshirika na mnufaika wa Mfuko wa Kusaidia Maendeleo ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) tangu Mwaka 2013 ambapo Awamu hii ya Tatu Serikali itanufaika kwa kupata Dola za Kimarekani 84.6 kutoka GPE sawa na Shilingi Bilioni 212.3 ambao afua zake zinajikita kuboresha mambo mbalimbali yanayohusu kada ya ualimu kwa muda wa miaka minne kuanzia mwaka wa fedha 2023/24 hadi 2026/27