Serikali imeanza kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, pamoja na Mitaala iliyoboreshwa kwa kuzingatia ujumuishwaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum ngazi zote za elimu.



Kauli hiyo imetolewa Septemba 20, 2024 jijini Arusha na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahera wakati akizungumza katika Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 30 ya Elimu Jumuishi, ambapo amesema utekelezaji wa Sera hiyo pia unaziangatia maadili, ujuzi, ubunifu na TEHAMA kwa Wanafunzi wote.



Amesema Wizara imeandaa miongozo inayoelekeza wadau wa elimu kushiriki katika mchakato wa utoaji wa elimu kwa usawa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.



"Tunajivunia mafanikio makubwa, tuna ongezeko la Wanafunzi walioandikishwa katika ngazi ya Awali, Msingi na Sekondari kutoka 3,789 mwaka 1997 hadi 97,305 mwaka 2024" alibainisha Mahera.



Vile vile Dkt. Mahera amesema kuwa walimu wa elimu maalum na jumuishi katika ngazi za Elimu Msingi wameongezeka kutoka 1,293 mwaka 1,997 kufikia 5,477 mwaka 2024.



Naibu Katibu Mkuu huyo ametoa wito kwa viongozi wa taasisi na wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha na kuchangia utekelezaji utoaji wa elimu kwa watu wenye mahitaji maalum