Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kimaghai ‘’A’’ Wilayani Mpwapwa umetokana na Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), na kwamba Wizara inaendelea kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila Kata ina shule ya Sekondari ifikapo mwaka 2027/2028.  

Waziri Mkenda amesema hayo Agosti 20, 2024 mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Phillip Mpango ambaye aliweka jiwe la msingi katika Shule hiyo iliyopo Kata ya Kimaghai wilayani Mpwapwa iliyogharimu Shilingi milioni 544.2.

‘’Na sera ambayo imepitishwa na sasa tunaisimamia, itakapofika mwaka 2027/28 ni kuhakikisha kila Mwanafunzi atakayemaliza Shule ya Msingi lazima aendelee kusoma mpaka kidato cha Nne" Alisema Waziri Mkenda.

Amesema kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI eneo ambalo lina Sekondari likitosha wataongeza shule ya Msingi ili sasa Tanzania Bara kila mtoto atakapoanza shule akiwa na miaka 6 atamaliza elimu ya lazima akiwa na miaka kumi na sita (16).