Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungango wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Mpango amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya Elimu kutoka na mabadiliko ya Sera na mitaala ya Elimu pamoja na maboresho ya miundombinu ya elimu.
Ameyasema hayo Agosti 13, 2024 Jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa Elimu wa Kikanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Sherehe za Mwaka wa Elimu wa Umoja wa Afrika 2024 uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Dkt Mpango amesema kuwa mataifa ya Afrika Mashariki yanapaswa kuongeza uwekezaji katika sekta ya elimu ili kukidhi mahitaji ya utoaji elimu bora.
Amesema hiyo inatokana na mwenendo wa ongezeko la idadi ya watu hususan vijana ambao wakipata elimu watakuwa na nguvu kazi yenye ujuzi na mahiri watakao shiriki katika kujenga uchumi.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu ambayo yanalenga kuongeza ubora wa elimu pamoja na kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi itakayoendana na mahitaji ya dunia ya sasa.
Akizungumza katika Mkutano huo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mkutano huo ni fursa nzuri kwa nchi za Afrika Mashariki kubalishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa mataifa mengine namna nzuri ya kuendeleza sekta ya Elimu.
Ameongezea kuwa Tanzania imeanza utekelezaji wa mageuzi katika ngazi zote za elimu na kwamba lengo kuu ni kuhakikisha taifa lina jenga nguvu kazi yenye ujuzi na umahiri.
Mkutano huo unahudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mawaziri wa Elimu na wawakilishi kutoka nchi wanachama za Afrika Mashariki, Wadau wa Maendeleo, Mashirika ya Kimataifa pamoja na Wadau wa Sekta ya Elimu.