Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema ni marufuku Mwanafunzi yeyote kufukuzwa kwenye shule za umma, kurudishwa nyumbani kwa sababu mzazi ameshindwa kuchangia mchango wowote ikiwemo huduma za chakula.
Mkenda ametoa agizo hilo Julai 26, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza katika Kongamano la Utoaji Chakula na Lishe Shuleni, akisisitiza mzazi anayekataa kuchangia mchango uliowekwa kulingana na miongozo waliyojiwekea Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaweza kuchukua hatua dhidi ya mzazi wakati Mwanafunzi akiendelea na masomo.
Akihutubia Kongamano hilo Waziri huyo amewataka Wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana kuhamasisha huduma ya chakula kwa Wanafunzi wakiwa shuleni.
"Lishe bora shuleni ni msingi muhimu katika maendeleo ya kiafya na kiakili na kwamba inachangia Mwanafunzi kujifunzaji kwa ufanisi. Mwanafunzi anapokosa chakula hukabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo njaa, utoro wa rejareja na hata kukatisha masomo kwa baadhi yao" alisema Mkenda