Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2024, Shule za Msingi za Serikali 854 zenye Wanafunzi 437,749 sawa na asilimia 70 ya Wanafunzi zimeweza kutoa huduma ya chakula Shuleni.



Aidha ameongeza kuwa Shule za Sekondari za Serikali 261 zimetoa chakula kwa Wanafunzi 143,700 sawa na asilimia 69.2 na kwamba Mkoa walau umepiga hatua japo juhudi zaidi zinaendelea kutekelezwa.



Mhe. Senyamule ameeleza Julai 26, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza katika Kongamano la Kitaifa la Utoaji wa Chakula na Lishe Shuleni na kusema kuwa katika kuunga mkono juhudi hizo Mkoa huo wameanzisha mpango wa kutenga maeneo ya mashamba na vitalu bustani Shuleni kuziwezesha Shule nyingi kupata chakula bora.



Ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kusimamia na kufuatilia suala la lishe Shuleni, hali inayochochea afya na elimu bora katika mkoa huo.