Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imetia saini makubaliano ya ushikirikiano na Taasisi ya Utafiti, Sayansi na Teknolojia ya Vignan's kutoka India.
Makubaliano hayo ni katika masuala ya Elimu, Sayansi,Teknolojia na Utafiti ikiwa ni pamoja na taasisi hiyo kupokea wanafunzi 100 kutoka Tanzania kila mwaka kwa ajili ya kusoma fani za kipaumbele ikiwemo Uhandisi ujenzi, Uhandisi Kilimo, Akili Mnemba, na Uhandisi wa Umeme kwa gharama nafuu.
Kamishina wa Elimu Dkt. Lyabwene Mutahabwa akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema bila Utafiti, Sayansi na Teknolojia ni vigumu kushindana popote.
Ameishukuru Serikali ya India na Taasisi ya Vignan's kwa utayari wa kushirikiana na Tanzania.
"ukiwa na rafiki ambaye yupo tayari kukusaidia kwenye eneo la Elimu kwenye nchi huyo ndiye rafiki wa kweli" amesema Lyabwene
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Vignan Srikant Nandigam amesema vijana wa Kitanzania watapata ujuzi na baada ya masomo watakuwa tayari kuajiriwa na kujiajiri pia hawatakaa India bali watarudi Tanzania kueneza ujuzi huo.
Amesema Taasisi ya Vignan's ina miaka 23 toka ianzishwe na kufanya kazi, huku ikiwa tayari imefanya kazi na mataifa 9 kutoka Afrika na Tanzania inakwenda kunufaika kwa mara ya Kwanza.
Tanzania ni Taifa la pili kwa kupeleka wanafunzi wengi zaidi nchini India baada ya Zimbabwe.