Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi chuo cha VETA cha Mkoa wa Rukwa kilichopo katika kijiji cha Kashai, Kata ya Momoka, wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, tarehe 16 Julai, 2024, ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Rukwa.
Mhe. Rais amesema kwa sasa mkoa wa Rukwa unakua kiuchumi, hasa katika eneo la miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo ni wakati wa vijana na jamii kwa ujumla kupata chuo cha kuwawezesha kupata ujuzi, utaalamu na maarifa ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko hayo makubwa ya kiuchumi.
"Chuo hiki ni jitihada za Serikali za kuhakikisha kwamba vijana na jamii yetu inatayarishwa na kupewa elimu ujuzi utakaowasaidia kujitegemea kwa kujiajiri au kuajiriwa," amesisitiza.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka msisitizo katika ujenzi wa vyuo vya VETA kote nchini na kuhakikisha kwamba kazi kubwa waliyopewa ya kuhakikisha Watanzania wanapata mafunzo ya ufundi stadi inatekelezwa kwa ufanisi.
Aidha Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa chuo hicho cha VETA cha Mkoa wa Rukwa, amesema ujenzi wa chuo hicho umefikia asilimia 90% na umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 6, ukiwa na jumla ya majengo 24 ambayo ni pamoja na Jengo la utawala 1, Nyumba za watumishi 3, Karakana 8, Jengo 1 la madarasa(General Classes), kibanda cha mlinzi 1, Nyumba ya Jenereta 1, Jiko na bwalo la kulia chakula 1, Maktaba 1, Mabweni 4 na Maabara ya kumpyuta 1.
CPA Kasore ameongeza kuwa chuo hicho kilianza kutoa mafunzo rasmi tarehe 18 Machi, 2024 kwa wanafunzi 63 wa fani mbili za Mafunzo ya muda mrefu za Umeme wa majumbani yenye wanafunzi 49 na Ubunifu wa nguo, ushonaji na teknolojia ya mavazi yenye wanafunzi 14.
"Pamoja na kozi hizi mbili (2) za muda mrefu tulizokwishaanza kuzitoa, tunatarajia kuongeza kozi nyingine 7 za Uashi, Uungaji na Uundaji vyuma, Ufundi Magari, Uhazili na Matumizi ya Kompyuta, Upishi, Useremala na Uchakataji wa Chakula ifikapo Januari 2025," ameongeza.