Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa Serikali yake italipa fidia ya Shs. Bilioni 1 na Milioni 7 kwa wananchi ili waachie eneo kwa ajili ya upanuzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Kampasi ya Mizengo Pinda Mkoani Katavi



Rais ametoa ahadi hiyo wakati akijibu hoja ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda Juni 15, 2024 katika mkutano wake na wananchi uliofanyika katika Kata ya Kibaoni, Halmashauri ya Mpimbwe.



Mhe. Pinda amesema, eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 240 au ekali 580 limekwama kuendelezwa na Chuo kutokana na kukosa fedha pamoja na kuwepo kwa juhudi zinazofanywa na Menejimenti ya Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo chini ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Chibunda.


"Kwa bahati nzuri Mhe. Rais hata Prof. Chibunda mwenyewe yuko hapa amekuwa akiweka jitihada kubwa namna ya kupata fedha ili eneo hili lifidiwe na litumike kujenga mabweni na madarasa kwa ajili ya wanafunzi"

Amesema Kampasi hiyo iliyopo chini ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo imekuwa mkombozi kwa wanachi wa ukanda huu kwani sasa watoto wanapata elimu hasa katika uzalishaji wa mazao, ufugaji wa nyuki na mazao yake lakini uhifadhi wa wanyama kutokana na kuwepo kwa hifadhi ya Katavi ambayo ina wanyama wakubwa kuliko maeneo mengine



Rais Samia akizungumzia hifadhi hiyo ameseme yeye mwenyewe atakuja kufanya Royal Tour sehemu ya pili katika hifadhi hiyo ambayo ameona ina wanyama wengi na wakubwa wanaovutia sana ili kufungua utalii katika eneo la ukanda huu.

Rais Samia amemaliza ziara ya siku nne katika mkoa wa Katavi ambapo amewapongeza viongozi na wananchi mkoani humo kwa kudumisha amani na kuwataka wahamiaji katika eneo kuhakikisha wanaendeleza amani waliyoikuta