Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema Tanzania imejiandaa kutumia Teknolojia kikamilifu katika kuimarisha ubora wa elimu na kuhakikisha inaendana na mahitaji ya soko la ajira Kimataifa na mahitaji mapana ya Taifa.
Prof. Nombo ametoa kauli hiyo Mei 28, 2023 jijini Tanga wakati akifungua Kongamano la Elimu, Ujuzi na Ubunifu linaloangazia masuala mbalimbali ya Elimu ikiwemo matumizi ya teknolojia katika nyanja mbalimbali pamoja na mikakati bora ya kuwianisha mifumo ya Elimu na mahitaji ya sasa.
"Tuna fursa ya kipekee ya kushiriki majadiliano haya muhimu juu ya masuala yanahusiana na mfumo wetu wa elimu, maendeleo ya ujuzi, na ujumuishaji wa sayansi, teknolojia na uvumbuzi" Alieleza Nombo.
Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu la Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Dkt. Adolf Rutayuga amesema wanayo furaha kuwaleta pamoja Washiriki mbalimbali, wakiwemo Wawakilishi kutoka taasisi za TVET, Taasisi za Elimu ya Juu, sekta binafsi, Washirika wa Maendeleo, na wadau wengine muhimu katika sekta ya elimu.