Tanzania ina hazina kubwa ya maarifa kutoka kwa viongozi watangulizi akiwemo Hayati Edward Moringe Sokoine.
Hayo yamesemwa April 8, 2024 na Mhe. Dkt. Dotto Biteko Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati akihutubia katika Kongamano la kumbukizi ya miaka 40 ya kifo cha Edward Moringe Sokoine lililoandaliwa na Chuo kikuu cha Sokione cha Kilimo ( SUA) Morogoro
Biteko amepongeza SUA na Wizara ya Elimu kwa kuendelea enzi fikra za Hayati Sokoine kwa kufanya mijadala na makongamano yanayoangalia mchango wake katika maendeleo ya Kilimo Nchini.
" nipongeze sana hatua ya kuwa na makongamano haya yanasaidia kujenga uelewa na kutoa historia ya kuongozi wetu mahiri na jinsi alivyochagiza maendeleo ya Kilimo ikiwemo kuanzishwa kwa Chuo hiki ambacho kimejikita katika mafunzo ya kilimo" , amesema Biteko
Biteko ameitaka Wizara ya Elimu na SUA kuhakikisha inaweka maandiko ya nasaha na hotuba za Hayati Sokoine kuhusu Kilimo na Maendeleo ikiwemo chambuzi mbalimbali zinazofanywa na Wanataaluma na Viongozi.
" leo hapa tulikua na wanazuoni nguli Prof Shivji , Prof Sibuga na Viongozi wetu Mhe Warioba na Mhe Anna Makinda , tumesikia uchambuzi juu ya Hayati Sokoine fikra, maono, na utendaji wake uliokuwa na weledi mkubwa ni vema hizi kumbukumbu zitunzwe"', Ameongeza Biteko
Amekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwa kuimarisha mafunzo kwa vitendo kwani inawajengea wahitimu ujuzi
Akizungumza katika Kongamano hilo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Vyuo Vyuo Vikuu nchini vitaendelea kufanya mijadala na chambuzi tunduizi kuhusu nyanja mbalimbali za maendeleo.
" tunaendelea kuweka msukumo katika mijadala na chambuzi za kitaaluma katika vyuo vikuu, mijadala hii inaelimisha na inatoa pia mawazo chanya kwa ajili ya maendeleo yetu", amesema Prof. Mkenda
Ameongeza kuwa taifa lina mengi ya kujifunza kutoka kwake katika Uongozi na jinsi alivyo chagiza maendeleo ikiwemo kufungua fursa mbalimbali za kilimo kibiashara.