Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Caloryne Nombo amewataka Wadau wa sekta ya Elimu kujadili kwa kina Mawasilisho na kutoa maoni yenye tija katika kuboresha Elimu nchini na kuchagiza Mageuzi katika sekta hiyo.
Ameyasema hayo leo Aprili 03, 2024 Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa pamoja wa Tathmini ya Sekta ya Elimu 2023, unaolenga kupitia na kuchambua Utekelezaji wa vipaombele vya mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu.
Aidha Katibu Mkuu huyo amewaeleza Wadau hao kuwa Wizara imefanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Elimu na kuanza utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na Mitaala mipya ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu.
Ameongeza kuwa maboresho ya Mitaala katika ngazi ya Elimu ya kati na Elimu ya Juu yanaendelea na kwamba Wadau mbalimbali watafikiwa ili kutoa maoni.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini, Dkt. Daniel Baheta ameahidi Serikali kuendeleza ushirikiano kuhakikisha Watoto wa kitanzania wanapata Elimu bora.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Elimu Tanzania, Tanzania Education Network (TENMET) Faraja Nyarandu amesema Mkutano huo utawasaidia kuja na mikakati ya kutatua changamoto mbalimbali kwenye Sekta ya Elimu.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Karibu Tanzania Organisation (KTO) Majid Mjengwa amesema wameendelea kushirikiana na Serikali kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) kwa kuhakikisha Wanafunzi kukatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito warejea Shuleni.