Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa, ili kuwe na mafanikio katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mitaala lazima kuwekeza katika kada ya Ualimu.
Prof. Nombo amesema hayo wakati akifungua kikao kazi kati ya Serikali, Shirika lisilo la Kiserikali la Mastercard Foundation na Wadau wa Sekta ya Elimu kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha kada ya ualimu kilichofanyika Machi 18, 2024 Jijini Dar es Salaam.
"Napenda Niwakumbushe kuwa, nchi yetu imeidhinisha toleo jipya la Sera ya Elimu na Mafunzo na pia ina Mitaala mipya ya awali, msingi, sekondari na ualimu, ili kuwe na mafanikio makubwa katika utekekezaji wake ni muhimu sana kuwekeza katika kuimarisha na kuandaa na walimu ambao ndio kitovu cha maarifa kwa wanafunzi.
Aidha, Prof. Nombo amesema, kikao hicho kinatoa fursa ya kubadilishana uzoefu kati ya nchi na nchi na kujadili ili mahitaji ya ualimu katika mwelekeo mpya wa elimu, changamoto na fursa za ushirikiano baina ya Shirika hilo, Wadau na Serikali ya Tanzania katika kuboresha mahitaji ya ualimu nchini.