# Tutaanza utalii katika Elimu
Na WyEST
Arusha
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua umuhimu wa Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya maendeleo ya nchi hivyo imewekeza miundombinu wezeshi katika Taasisi za kielimu zilizojikita katika nyanja hizo ikiwemo Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Professa Carolyne Nombo Desemba 14, 2023 Jijini Arusha wakati wa ziara yake ya kikazi katika taasisi hiyo ili kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Profesa Carolyne amesema, Serikali inawekeza zaidi katika eneo la kibiashara kuhakikisha kwamba Teknolojia zote zilizozalishwa na watafiti zinaingia sokoni kwa kuangalia mazingira ya biashara kupitia kampuni zke tanzu na kwa kushirikisha wadau.
“Kupitia costech serikali huwa inatenga fedha kila mwaka kuwezesha kuboresha Teknolojia zilizozalishwa na watafiti wetu na wabunifu mbalimbali ili kuzifikisha katika hali ambayo inafaa kuingizwa sokoni kwa ajili ya kutatua changamoto za kijamii”
Aidha, Professa Carolyne aliongeza kuwa sekta ya elimu ina ajenda ya kufanya utalii wa elimu kwa kuwavutia watu mbalimbali kuweza kutembelea Taasisi za elimu ili kujifunza masuala ya bunifu na Teknolojia mbalimbali zilizopo zinazowezesha sekta mbalimbali.
“Wengi wetu wakienda nje ya nchi wanapenda kufanya utalii kwenye vyuo vya elimu au Taasisi za utafiti tunataka na sisi Tanzania tuwezeshe utalii wa kielimu na hivyo kuongeza idadi ya watalii watakotembelea nchi yetu” alisema Professa. Carolyne Nombo
Naye Makamu Mkuu wa Taasisi Prof. Maulilio Kipanyula ameeleza kuwa, lengo la ziara ya Katibu Mkuu Professa Carolyne ni kujionea utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazotokelezwa na Taasisi hiyo kwa kutembelea Maabara za kufundishia na Utafiti pamoja na Kituo cha Atamizi kuona bunifu mbalimbali zinazozalishwa.