Wasimamizi wa mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Elimu ya Juu (HEET) kutoka katika Taasisi na Vyuo Vikuu 22 washiriki mafunzo ya wanajengewa uwezo kukabiliana na vihatarishi katika kutekeleza mradi huo ili kupunguza athari na kutimiza malengo ya mradi.

Mafunzo hayo ya siku tano yanafanyika katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ambayo yameanza tarehe 4 na yanatarajiwa kukamilika Disemba 8, 2023 Jijini Arusha chini ya uratibu wa Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia.



Mratibu wa Mradi huo Ngazi ya Kitaifa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Kenneth Hosea amezitaka Taasisi na Vyuo Vikuu vinavyotekeleza mradi huo kuzingatia mafunzo hayo kwa kuwa ni muhimu katika utekelezaji ili kujua vihatarishi na kuvipunguza.



Dkt. Sako Mayrick mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Fedha ameeleza umuhimu wa kujua vihatarishi vya ndani na nje kwa kuzingatia malengo ya mradi kwa ngazi ya Kitaifa na Kimataifa , pamoja na aina za vihatarishi na sifa za vihatarishi

"Ni muhimu kuelewa mradi una malengo gani na maeneo ya kuzingatia jambo ambalo litatoa mwanga wa kujua vihatarishi na kuweza kuvishughulikia" amesema Dkt. Sako.



Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi Mipango, Fedha na Utawala Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela na Mradi wa Taasisi Prof. Suzana Augustino kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Taasisi Prof. Maulilio Kipanyula amewakaribisha washiriki na kuwatakia mafunzo mema yenye kuleta tija katika kutekeleza mradi.