Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amezitaka Taasisi za Vyuo Vikuu Barani Afrika kuendelea kushirikiana katika kuimarisha ubora wa Vyuo Vikuu.

Prof. Mkenda ametoa rai hiyo Novemba 28, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa Mtandao wa Wadhibiti Ubora Barani Afrika (AfriQAN) unaoshughulikia masuala ya ubora katika elimu ya Juu, udhibiti na Usimamizi.

"Shinikizo la kushusha ubora siku zote lipo, tusikubali kwa nama yoyote ile, lazima sisi tuhakikishe tunapima ubora wa Vyuo Vikuu kwa namna vinavyoweza kumuandaa Mhitimu kuweza kuajiajiri ama kuajiriwa kirahisi" Alisema Prof. Mkenda



Pia amezihimiza Taasisi hizo kuzingatia suala la maadili na weledi katika uendeshaji na Usimamizi wa Vyuo hivyo hasa katika kutoa huduma Bora kwa jamii ili kukabiliana na ushindani katika Elimu.

"Uendeshaji wa Vyuo Vikuu ni biashara yenye ushindani makubwa, na katika ushindani huo pasiwepo na nguvu ya ushawishi ya kushusha viwango ili kupata sifa ya kuwa na maprofesa wengi, viwango hivyo ni lazima viwe vya Kimataifa kwa Afrika nzima" alibainisha Waziri Mkenda.



Nae rais wa Mtandao wa Wadhibiti Ubora Barani Afrika (AfriQAN) Prof. Maria Luisa Chicote amesema Mkutano huo unadhamiria kujadili fursa mbalimbali za namna ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika Vyuo Vikuu pamoja na kujadili juu ya madhara ya changamoto za kidigitali zinazoathiri ubora elimu ya Juu.



Akizungumza manufaa ya Mtandao huo Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof. Charles Kihampa amesema u ulianzishwa tarehe 27 Novemba 2009, na kwamba kwa mara ya kwanza mkutano huo unafanyika nchini Tanzania, lakini ni mkutano wa 14 na umekuwa ukifanyika katika nchi mbalimbali.



"Mtandao wa Wadhibiti Ubora Barani Afrika ni muhimu kwa sababu tunashirikiana na Wadhibiti ubora wa nchi mbalimbali katika kudhibiti Ubora wa Elimu, kuanzia ya Msingi mpaka Vyuo Vikuu" alieleza Prof. Kihampa.

Aidha Kihampa ameongeza kuwa mkutano wa leo umeshirikisha nchi 22 kutoka Afrika na nchi tatu Nje ya Afrika ambazo tunashirikiana katika kuandaa taratibu mbalimbali za uendeshaji wa Taasisi za elimu ya Juu.