Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayans i na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amewataka watafiti katika Vyuo Vikuu nchini kutambua kuwa wanawajibu wa kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Katibu Mkuu amesema hayo wakati akifungua zoezi la utoaji wa zawadi kwa Wanachuo, Watafiti na Viongozi wa Chuo waliofanya vizuri kwenye masomo katika Ndaki mbalimbali za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Prof. Nombo amesema Chuo ni sawa na Kiwanda kama Hayati Mwalimu Julius Nyerere alivyosema, Chuo ni kama Kiwanda kwa sababu kinazalisha wataalamu wanaopaswa kutumia utaalamu wao kwa manufaa ya jamii hivyo kuonesha umaana wa elimu.
Alisema majukumu ya Vyuo Vikuu ni kufundisha, kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kuzifikia jamii na kwamba kwa kupitia matokeo ya tafiti ndipo jamii itafikiwa kwa kutumia matokeo ya tafiti hizo kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Naye mmoja wa watafiti aliyepata tuzo ya mtafiti bora wa mwaka kutoka Kampasi ya Tiba ya Wanyama na Sayansi Afya, Profesa Robinson Mdegela amesema amefanikiwa kupata tuzo hiyo baada ya kufanya tafiti yenye kugusa maisha ya Watanzania ikiwemo kupambana na ongezeko la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa tatizo linalokaribia kuua watu karibu 12500 kwa mwaka kiwango ambacho ni karibu mara 10 ya idadi inayosababishwa na malaria au UKIMWI.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amesema kwa mwaka huu 2023 wamefanikiwa kutoa zawadi 248. Tuzo hizi hutolewa kila Mwaka ili kuweka ushindani unaochagiza mabadiliko chanya
Prof. Chibunda amesema mabinti wanaonekana kuwa mstari wa mbele katika kupata zawadi na kuongezeka kila mwaka jambo ambalo linaashiria wanazidi kuongeza juhudi ya kusoma na kuweka changamoto kubwa kwa wanafunzi wa jinsia ya kiume.
Naye mwanafunzi aliyepata tuzo tatu ikiwemo ya mwanafunzi bora wa kike na pia mwanafunzi bora mwaka wa tatu kwa Shahada ya Usimamizi wa Nyuki na Rasilimali zake Vaileth Chiwango alisema atatumia tuzo hizo kubadilisha jamii hasa inayofanya ufugaji wa nyuki kizamani kwa kuwawezesha kutumia mizinga ya kisasa na kusimama ufugaji kimaendeleo.