Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Husna Juma Sekiboko, amekipongeza Chuo cha Ufundi Arusha kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Nishati Jadidifu katika kampasi ya kikuletwa.
Kampasi hiyo iliyopo Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro, kupitia ufadhili wa mradi wa Ujuzi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EASTRIP) inajenga miundombinu mbalimbali ya kufundishia na kujifunzia.
Akizungumza mara baada ya ziara ya Kamati katika Kampasi hiyo ambayo inajengewa miundombinu ya madarasa, karakana, mabweni pamoja na ukumbi wa mihadhara ameitaka Wizara kuangalia namna bora ya kuongezea nguvu mradi huo ili ukamilike kwa wakati.
“Kimsingi tumetembelea maeneo mengi tumejionea wenyewe kile ambacho ATC mnatekeleza, niwapongeze kifupi mnafanya vizuri, viwango ni vizuri, tunaridhika na utekelezaji wa mradi unakwenda vizuri ,” alisisitiza Mhe. Sekiboko
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga, ameishukuru Kamati hiyo kwa kutembelea Chuo cha Ufundi Arusha, Kampasi ya Kikuletwa, na kuahidi Wizara itatekeleza maoni, ushauri, mapendekezo na maagizo yote ya kamati ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Akiwasilisha taarifa ya Chuo kwa Kamati, Mkuu wa Chuo Dkt. Musa Chacha amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 62 ambapo ukikamilika utakuwa nna manufaa makubwa katika kuongeza nguvu na wataalamu wa sekta ya Nishati.