Benki ya Dunia imeipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kusimamia na kutekeleza Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ufanisi mkubwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Oktoba 24, 2023 katika kikao cha pamoja cha kuanza kufanya tathimini ya utekelezaji wa Mradi wa HEET kati ya Benki hiyo na Wizara, Kiongozi wa Timu ya Ufundi ya Benki ya Dunia Roberta Mallee Basset, amesema katika kipindi cha miezi sita iliyopita inaonekana juhudi kubwa inayofanywa na wizara katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo.
"Niwapongeze Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi zote zinazotekeleza Mradi wa HEET kwani wameonyesha juhudi kubwa katika kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi kwani upo katika hatua nzuri " amesema Bassett.
Ameongeza kuwa kwa kawaida Benki ya Dunia imekuwa na utaratibu wa kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi kila baada ya miezi sita ambapo watatembelea maeneo mbalimbali ili kuona namna Mradi unavyotekelezwa na kubaini iwapo kuna changamoto ya aina yoyote ili kwa kushirikiana itatuliwe.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kusaidia katika Sekta ya elimu ambayo imekuwa katika kuboresha hali ya utoaji elimu, kuongeza fursa n za kuhakikisha elimu inatolewa nchini ni bora.
Prof. Nombo amesema Serikali itahakikisha inasimamia kwa ufanisi utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo katika Sekta ya elimu ili iwe na tija kwa nchi na kusaidia upatikanaji wa elimu bora kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na Mradi wa Kuongeza Fursa za Upatikanaji wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST), Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na Mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ) ambayo yote inalenga katika kuboresha na kuongeza fursa za elimu.
" Utekelezaji wa miradi yote tutahakikisha inakwenda sambasamba na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023" amesisitiza Prof. Nombo
Katibu Mkuu huyo amewataka wanaosimamia Mradi wa HEET kuhakikisha wanaendelea kusimamia mradi huo kwa weledi ili kuukamilisha kwa viwango na kwa wakati,huku akiahidi kuhakikisha inakuwa na wataalamu wanaohitajika.
Katika kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa HEET watatembelea Chuo Kikuu cha Sayansi Mbeya, Chuo Kikuu Ardhi na pia watapata nafasi ya kutembelea shule za Msingi na Sekondari Mbeya na kuongea na Wanafunzi na Walimu.