Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kazi kubwa inayofanya katika kuhakikisha nchi inakuwa na Sera na Mitaala itakayowezesha watanzania kupata elimu bora.
Ametoa pongezi hizo Oktoba 16, 2023 Mkoani Tanga wakati akifungua Mkutano wa 32 wa Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo ambapo amewataka watumishi hao kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa bidii, weledi na nidhamu ilikuleta ufanisi katika kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa katika viwango vya ushindani kitaifa, kikanda na kimataifa
Mkuu wa Mkoa huyo pia amewataka wajumbe wa baraza hilo kuhakikisha wanatekeleza maazimio yote waliyokubaliana katika mkutano kwa kusimamia na kushiriki ipasavyo katika hatua za utekelezaji wa Sera na Mitaala iliyohuishwa ili ilete tija na kuendana na kasi ya maendeleo ya elimu, sayansi na teknolojia duniani.
"Ndugu zangu dunia inapiga kasi sana hasa kwenye eneo la sayansi na teknolojia, mkatusaidie kwa kuhakikisha yale yanayofundishwa yanaendana na ukuaji wa sayansi na teknolojia, Siku hizi kuna akili bandia je tumewaandaaje watoto katika hili? " amesisitiza Mkuu wa Mkoa
Mhe. Kindamba ameongeza kuwa ni lazima wizara kuhakikisha vijana wanakuwa na uwezo, maarifa, stadi na umahiri katika ubunifu utakaowawezesha kuingia kwenye ushindani wa soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amesema kuwa wajumbe wa baraza hilo wana wajibu wa kusimamia na kuhakikisha dira, dhima na majukumu ya wizara yanatekelezwa kwa ufanisi ili kufikia malengo ya serikali katika sekta ya elimu.
Prof. Mdoe ameendelea kueleza kuwa mkutano pamoja na mambo mengine una jukumu la kujadili utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo ya Mwaka wa Fedha 2023/24, kujadili changamoto zilizopo na kutafuta ufumbuzi.
Naye Kaimu Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Suzan Lushinde amesema kuwa mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe 96 kutoka idara na vitengo vya wizara, Halmashauri za vyama vya wafanyakazi, viongozi wa TUGHE na CWT kanda na Taifa