Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amewataka maafisa wanaosimamia madawati ya mikopo katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini kutoa huduma bora kwa wanafunzi.

Prof. Mdoe ametoa wito huo leo Oktoba 11, 2023 wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu kati ya Menejimenti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na maafisa mikopo kutoka taasisi 80 zenye wanafunzi wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

“Huduma tunayowapa wanafunzi wa elimu ya juu wanaopokea mikopo siyo hisani, ni haki yao. Ninajua mnatoa huduma nzuri, lakini kuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi" Prof. Mdoe amewaambia maafisa zaidi ya 100 wanaohudhuria kikao kazi hicho kinachofanyika mjini Bagamoyo, Pwani.

Pamoja na wito huo kwa maafisa, Prof. Mdoe amezitaka menejimenti za taasisi za elimu ya juu kuimarisha ofisi zinazozosimamia mikopo ya wanafunzi vyuoni kwa kuteua maafisa wenye uwezo, kuwapa vitendea kazi na kuwajengea uwezo ili waweze kutoa huduma bora kwa wanafunzi.

“Wakuu wa taasisi za elimu ya juu wawawezeshe maafisa wanaosimamia mikopo vyuoni, wapewe vifaa na wajengewe uwezo, ni muhimu kujua kuwa pamoja na kutoa huduma, lakini takribani asilimia 60-70 ya mapato ya vyuo vingi yanatokana na fedha za mikopo, wawezeshwe,” amesisitiza Prof. Mdoe.



Awali akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB Prof. Hamisi Dihenga amesema kila mwaka, kabla ya kuanza kwa mwaka wa masomo, HESLB huandaa kikao kazi na maafisa mikopo kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo ili kutoa huduma bora kwa wanafunzi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema kikao kazi hicho kinaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Umuhimu wa TEHAMA katika kuboresha huduma kwa wanafunzi’ na kuwa maafisa mikopo wanaohudhuria watafundishwa kuhusu mifumo ya TEHAMA iliyoboreshwa.



Frida Malya, Ofisa Mikopo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Maafisa Mikopo hao amewakumbusha wanafunzi kufuata taratibu wanapokuwa vyuoni ili kuwezesha kupata huduma kwa wakati