Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya mkutano na Wamiliki wa Shule zisizo za Serikali kwa lengo la kusikiliza na kujadiliana kwa pamoja changamoto zilizopo katika sekta hiyo.
Akizungumza Oktoba 10, 2023 jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mkutano huo ni wa Kihistoria kwani kwa mara ya kwanza unafanyika ikiwa ni ushirikishwaji wa Sekta Binafsi na unalenga kusikiliza changamoto katika uwekezaji, uendeshaji wa shule na kuona namna ya kusaidia kuzitatua na kuweka mikakati ya pamoja.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa kusaidia kutatua changamoto zilizopo katika sekta binafsi na taasisi zisizo kuwa za serikali ambazo zinatoa huduma katika sekta ya elimu ni kutasaidia kuchangia utoaji elimu bora kwa watoto wa kitanzania.
"Ninaamini baada ya mkutano huu tutakuwa na mstakabali mzuri kwa ajili ya maeneleo ya elimu yetu, hivyo tunawataka muongee bila uoga tupo hapa kuwasiliza ili tukitoka hapa tuwe tumejipanga vizuri zaidi kuhakikisha tunaboresha elimu yetu" amesema Prof. Mkenda.
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga amesema kuwa majukumu ya serikali katika elimu ni kuhakikisha inatoa elimu kwa wote hivyo sekta binafsi na taasisi nyingine zinaisaidia serikali katika jukumu hilo.
Mkutano huo pia umehusisha Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi ajira Vijana na Watu wenye ulemavu ambapo Mhe Patrobas Katambi alishiriki. Wengi ni kutoka Wizara ya Ardhi na Makazi, NECTA na TET.