# Bilioni 48 zatengwa 
# 2023/24 wanafinzi 800 kunufaika

Serikali imetenga Sh 48 bilioni kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi 8000 wa ngazi ya stashahada katika fani mbalimbali za kipaumbele nchini kwa mwaka wa masomo 2023/24

Akizindua mwongozo wa utoaji mikopo hiyo jijini Dar es Salaam Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema ni dhamira ya serikali kuona vijna wengi wanapata elimu ya ujuzi na kushiriki katika ujenzi na Maendeleo ya Taifa.

Ametaja fani za kipaumbele ambazo zitagharamiwa kuwa ni pamoja na Afya na Sayansi Shirikishi, Ualimu, usafiri na Usafirishaji, Uhandisi Nishati, Madini, Sayansi na Ardhi pamoja na Kilimo na mifugo.

Amewataka waombaji wa mikopo hiyo kusoma Mwongozo  unaopatikana katika tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  (www.moe.go.tz),  Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu (www.heslb.go.tz) na  NACTVET  www. nactvet.go.tz  kuanzia leo Oktoba 4, 2023.

" Niwaombe waombaji wa mikopo kusoma mwongozo na kuuelewa, tusingependa kuona mwanafunzi mhitaji anakosa mkopo kwa sababu ya kukosea kuomba, "amesema Prof. Mkenda

Akizungumzia mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika katika kuboresha elimu ya Juu Prof. Mkenda amesema  ni kuongezeka kwa bajeti ya mikopo ya wanafunzi kutoka Bilioni 570 mwaka 2021-2022 hadi kufikia bilioni 731 mwaka 2023-2024, kuanzishwa kwa Samia "Scholarship" ambapo huu ni mwaka wa pili na Serikali imetenga Bilioni. 6.7 kwa ajili ya wanafunzi 1200.

"Ilani ya Chama cha Mapinduzi ( 2020-2025) Ibara 80 Ukurasa wa 127 - 131 inaeleza Malengo ya Serikali katika sekta ndogo ya elimu ya Juu kuwa itaimarisha na kuboresha mfumo wa ugharamiaji wa Elimu ya Juu ikiwemo Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji na sifa stahiki wanapata fursa ya kujiunga na elimu ya juu,"amesema Prof. Mkenda

Na kuongeza "Tuna lengo la kupanua wigo wa ufadhili wa samia, kukuza mfuko wa fedha  kwa kukaribisha wadau wengine waweze kuchangia". 

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Rehema Madenge ameipongeza Serikali kwa kutoa mikopo hiyo na kusema kuwa inatoa fursa kwa vijana  walio wengi kupata ujuzi na hatimaye ajira.

Nae  Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu Prof. Hamis Dihenga amesema hatua ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashada katika eneo la Amali ni kubwa katika kujenga vijana wenye ujuzi na kwamba Bodi hiyo na  Menejimenti ya bodi ipo tayari kuhakikisha kazi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu  ya Juu Bw. Abdul - Razak Badru amesema Muongozo huo umeandaliawa na  Wataalamu kutoka Wizara ya Elimu ya Elimu, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na kushirikisha sekta na Wizara mbalimbali katika kutambua fani za kupaumbele na programmu zenye uhitaji  wa wataalamu.