Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Wizara pamoja na Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu vya Umma katika kikao kilichojadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya Elimu ya Juu Nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amevitaka Vyuo vikuu kuimarisha ushirikiano na sekta mbalimbali ambazo wanaandaa watalamu wake. Avitaka kuandaa wataalamu wenye ujuzi
Amesema hayo Septemba 29, 2023 Jijini Dar es Salaam katika kikao chake na Makamu wa Wakuu wa Vyuo Vikuu vya Umma nchini ambapo alipokea taarifa ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha Elimu ya Juu nchini na kupongeza hatua kubwa ya uboreshaji miundombinu na mafunzo.
Rais amevitaka Vyuo Vikuu kuongeza Ubora wa mafunzo ili kutoa wahitimu wanaokidhi soko la ajira la Kitaifa, Kikanda na Kimataifa katika sekta mbalimbali.
Amevitaka Vyuo hivyo katika mafunzo kuzingatia mipango ya maendeleo ya nchi na kujikita katika kufanya tafiti zenye tija na ubunifu katika maeneo huku akitolea mfano mpango wa BBT katika kilimo na mifugo na kusisitiza ushirikiano na Taasisi za utafiti na maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amemshukuru Rais kwa kuipa kipaumbele sekta ya Elimu na kueleza kuwa wakuu hao wa vyuo awali walikutana na Katibu Mkuu kiongozi ambapo baada ya mazunguzo tayari changamoto mbalimbali zilizoibuliwa zimeanza kupatiwa ufumbuzi.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya Vyuo ili kuongeza udahili katika vyuo vikuu na kuvitaka vyuo hivyo kuhakikisha vinapanua wigo wa Mapato na kutenga asilimia 40 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuendeleza miundombinu.
Prof. Mkenda amesisitiza kuwa pamoja na Serikali kukamilisha mageuzi makubwa katika Elimu Msingi na Ualimu, kwa upande wa Elimu ya Juu uwekezaji mkubwa umefanyika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kampasi 14 mpya za Vyuo vikuu nchini kupitia mradi wa HEET. Amesema katika kutambua mahitaji ya ujuzi kampasi hizo zitajikita katika kutoa mafunzo ya ujuzi na kuimarisha tafiti katika sekta mbalimbali za kipaumbele.
Mkenda ameongeza kuwa uwekezaji unaofanyika unaenda sambamba na uandaaji wa Watumishi ikiwemo Wahadhiri ambapo kupitia mradi huo zaidi ya Wahadhiri 342 kutoka Vyuo vya Umma na Binafsi wamepelekwa masomoni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Vyuo Vikuu na Marasi wa Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma Tanzania Prof. Evaristo Liwa akisoma taarifa ya Wakuu wa Vyuo katika kikao cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu vya Umma nchini Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 29, Septemba 2023.
Prof. Liwa amemshukuru Rais kwa mageuzi makubwa na maendeleo yanayofanyika katika Vyuo Vikuu.
Ametaja baadhi ya mafanikio kuwa ni ongezeko la bajeti ya Wizara, ongezeko la mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kutoka bilioni 464 Mwaka 2020/21 hadi bilioni 739 Mwaka 2023/24 na hivyo kulngeza idadi ya kufikia 202,016 mwaka 2022/23.
Mafanikio mengine ni ongezeko la udahili wa Wanafunzi katika Vyuo Vikuu, maboresho ya Mitaala na kuongeza mitaala mipya, ambapo Vyuo vinaendelea kuboresha mitaala hiyo ili kuendana na maboresho ya Sera ya Elimu na mabadiliko ya Mitaala ya Elimu Msingi.
.