Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula ameutaka Uongozi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Gera kufanya tafiti mbalimbali za kilimo pamoja na ufugaji Nyuki.
Ameyasema hayo leo September 13, 2023 alipotembelea Chuo hicho kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa pamoja na kukagua ukarabati na ujenzi wa majengo mapya Chuoni hapo.
Rwezimula ameongeza kuwa ni muhimu kwa Chuo kufanya uchunguzi wa aina za mazao yanayoota vizuri katika ukanda huo na kutoa mafunzo juu ya kilimo hicho na uchakataji mazao yake.
"katika eneo hili chuo kijikite katika mafunzo ya kilimo, fanyeni tafiti na mtoe mafunzo juu ya kilimo kinachofaa hapa pamoja na mafunzo ya uchakataji mazao yake" amesema Rwezimula.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Gera Kagera Shomary Lugome amesema Chuo kinaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwezesha ukarabati pamoja na vifaa vya mafunzo.
Amesema ukarabati huo umewezesha Chuo kuongeza wigo wa kudahili kutoka Wanachuo 45 kabla ya ukarabati 2018 hadi kufikia Wanachuo 310 baada ya ukarabati.
Ameongeza kuwa wanajivunia kuwa vijana wahitimu wa Chuo hicho wanatoka na ujuzi na kuwa Chuo kinawafutilia na idadi kubwa wameajiriwa na kujiajiri.