Kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu Utamaduni na Michezo imeshauri Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha inawekeza vifaa muhimu vya kujifunzia katika Chuo cha VETA Kagera ili kuunga mkono maono ya Rais Dkt. Samia Suluh Hassan ya kuwekeza katika kutoa ujuzi.
Agizo hilo limetolewa na mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Husna Juma Sekiboko aliyeongoza kamati hiyo na kutembelea na kukagua shughuli za ufundishaji na ujifunzaji katika Chuo hicho.
Ametumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Dkt. Samia Suluh Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwekeza fedha nyingi kwenye ujenzi wa vyuo vya Veta nchini ili kuweza kuwasaidia watanzania walio wengi kuwa na ujuzi.
Ameitaka wizara ya elimu kuyaishi maono hayo kwa kuongeza zaidi mafunzo ya vitendo hivyo kuhitaji kuongeza uwekezaji kwenye vifaa.
Akiongea katika ziara hiyo mjumbe wa kamati Mhe. Mwalimu Aloyce Kamamba ameipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa wa chuo cha Veta Kagera na kusema kuwa kwenye vyuo vya VETA ndiko kutapatikana mafunzo ujuzi wa kumaliza changamoto wananchi na kuongeza kuwa serikali iendelee kuwekeza vifaa pamoja na wahitimu kupewa fedha kama mtaji.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Elimu sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga amesema kuwa wizara imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na kamati na kuaahidi kuyafanyia kazi kwa haraka ili kutimiza malengo ya serikali ikiwemo kuendeleza nabkukamilisha ujenzi wa Vyuo 64 vya VETA.
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma kwenye chuo hicho wameishukuru serikali kwa kujenga chuo hicho ambacho kimetoa fursa kwa vijana ambao walikuwa vijijini na sasa wanapata ujuzi huku wengine wakiomba serikali kutoa fursa ya vijana hao kupata mikopo ili kuweza kupunguza ukali wa maisha hasa wawapo chuoni.
Chuo cha Veta Kagera kilichojengwa kwa ufadhili wa serikali ya China kwa gharama ya shilingi bilioni 22 katika kata Nyakato Halmashauri ya wilaya Bukoba kina uwezo wa kuwahudumia wanafunzi 400 fani za muda mrefu na 1000 fani za muda mfupi