Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema msisitizo wa Serikali ni kuhakikisha mazingira ya utoaji elimu nchini yanakuwa bora na kuhamasisha ushiriki wa kila mdau kuchangia kwenye sekta ya elimu.
Prof. Nombo amesema hayo jijini Dar es Salaam alipokutana na baadhi ya wanachama wa Mtandao wa elimu Tanzania (TENMET) na kutoa shukrani za Serikali kwa wadau wote wanaoendelea kuchangia kwenye Sekta ya elimu.
“Tunawashukuru sana kwa namna mnavyowekeza kwenye elimu, niwaombe katika utekelezaji wa majukumu yenu muyafikie maeneo ambayo hayajafikiwa badala ya kupeleka eneo moja mahitaji yanayofanana isipokuwa yanatekelezwa na wadau wawili tofauti,”amesema Prof. Nombo.
Pia amewaomba wadau hao pamoja na kuwa moja ya lengo lao ni kuhakikisha elimu ya mtoto wa kike, kuangalia pia watoto wa kiume kwa kuwa kumekuwa na mdondoka wa watoto hao kwenye elimu.
Akizungumzia mageuzi ya elimu nchini Prof. Nombo amewaomba wadau kuungana na Serikali kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mtaala mpya kulingana na Sera mpya ikipitishwa unafanyika kwa ubora.
“Nimeambiwa mmeshiriki katika michakato mbalimbali ya mabadiliko ambayo yanaendelea katika Sekta, ninyi ni sehemu ya mabadiliko hayo. Ukweli ni kwamba kulingana na kalenda za Serikali zitakaporuhusu na idhini tutakayopewa na Baraza la Mawaziri tunapanga kuanza utekelezaji wa mtaala mpya mwaka 2024 tumetenga sehemu ya bajeti kwa ajili ya kuanza utekelezaji huo lakini bado tunahitaji wadau wengine wengi,” amesema Prof. Nombo
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET) Ochola Wayoga amesema katika utekelezaji wa majukumu yao wataendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha elimu ya mtoto wa kitanzania inakuwa bora huku Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu Dkt. John Kalaghe akisema kitendo cha kutembelewa na kiongozi huyo kimewatia moyo na kwamba wataendelea kutoa taarifa za utekelezaji kwa kazi wanazozifanya.