Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema serikali inaendelea kufanya uwekezaji na uboreshaji wa miundombinu kuhakikisha inaongeza ufaulu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo Septemba 5, 2023 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma kuhusu mikakati inayotekelezwa na Wizara katika kuinua kiwango cha ufaulu wa masomo hayo.
Prof. Mkenda amesema pamoja na jitihada hizo Wizara inatambua umuhimu wa masomo hayo na ipo tayari kuunga mkono mapendekezo mbalimbali ya Viongozi pamoja na Wadau yanayolenga kujadili mikakati ya pamoja kwa ajili ya kutatua changamoto ya ufaulu hasa somo la Hisabati.
‘’Hakuna nchi yoyote duniani inaweza kuendelea bila kufanya uwekezaji wa kutosha katika Sayansi na Teknolojia, Hisabati ni roho ya masomo hayo, na kama tunataka kuandaa kizazi chenye Wataalam mahiri, lazima tuwe na ufaulu mzuri wa Sayansi na Hisabati’’. Alisema Prof. Mkenda.
Aidha amesema katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu, serikali tayari imeajiri Walimu wa Sayansi takribani Elfu Kumi, pamoja na kutoa mafunzo kwa Walimu zaidi ya elfu 22 kupitia Mafunzo Endelevu kwa Walimu Kazini (MEWAKA)"
‘’Vile vile tunawekeza zaidi katika ujenzi wa maabara pamoja na kununua vifaa vya maabara kuanzia shule za Sekondari hadi Vyuo vya Ualimu, kuhakikisha ufundishaji wa masomo ya Sayansi unafanyika vizuri’’ alibainisha Prof. Mkenda
Waziri Mkenda ameongeza kuwa ili kuhamasisha wanafunzi katika masomo ya Sayansi, serikali imeanzisha Samia Skolashipu inayo wahakikishia vijana wa Kitanzania wanaomaliza Mtihani wa kidato cha Sita na kufaulu vizuri tahasusi za Sayansi kusomeshwa na serikali, endapo watakwenda Vyuo vikuu kuendelea kusoma masom ya Hisabati, TEHAMA, Uhandisi na Elimu Tiba.
'’Aidha tumeweka tuzo ya Wahadhiri wa Masomo ya Sayansi ambao watakuwa wanachapisha Matokeo ya utafiti wao kwenye majarida makubwa na maarufu duniani, ukifanya vizuri unapata kitita cha shilingi milioni 50 kwa kila chapisho, na hivi karibuni tutaanza kutoa tuzo hizo’’. Alifafanua Prof. Mkenda