#JK atoa wito kukamilisha ahadi hizo
#Aeleza namna Tanzania ilivyonufaika zaidi na GPE
Tanzania kwa awamu mbili tofauti imenufaika na Mfuko wa kusaidia maendeleo ya elimu duniani kuanzia mwaka 2014 hadi sasa kwa kiasi cha sh bilioni 518.8 ambazo zimeelekezwa kwenye miradi ya elimu ya msingi.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ambae pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya GPE Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo kwenye Hafla ya Kutambu Mchango wa Wadau wa Sekta ya Elimu mkoani Dar es Salaam.
Dkt. Kikwete amesema awamu ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2014 hadi 2018 na ya pili ni mwaka 2019 hadi 2023.Alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na fedha hizo katika awamu ya pili kuwa ni ujenzi wa madarasa ya shule za msingi 2,980, ujenzi wa matundu ya vyoo 7,673, nyumba za walimu 64, shule mpya 18 na mabweni ya wanafunzi wenye mahitaji maalum 15.
Mengine ni ujenzi wa madarasa ya mfano ya elimu ya awali 300, ukarabati wa shule zenye vitengo vya elimu elimu maalum 13 na ujenzi, ukarabati na ununizi wa vifaa kwa vituo vya walimu 252.
“Uboreshaji wa miundombinu hii umewezesha serikali kuimarisha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji shuleni kuendana na ongezeko la idadi ya wanafunzi,” amesema Mhe. Kikwete
Alisema ufadhili wa GPE pia umewezesha upatikanaji wa jumla ya nakala za vitabu 36, 118,566 zilizochangia kuimarisha ubora wa elimu katika ngazi mbalimbali za elimu ya msingi kwa kuimarisha ujifunzaji na upatikanaji wa maarifa.
Vilevile ufadhili huo umesaidia kuimarisha mfumo wa kutathimini ubora wa shule kwa ngazi ya awali na msingi pamoja na kusaidia utekelezaji wa mpango wa mafunzo endelevu kwa walimu kazini ambao umekuwa ni nyenzo muhimu katika kuimarisha utendaji wa kuboresha matokeo ya ujifunzaji kwa wanafunzi nchini.
Akizungumzia ahadi ziliotolewa na Wakuu wa Mikoa Mhe. Kikwete ametoa rai kwao kuhakikisha wanakamilisha ahadi hizo za zaidi ya Sh Bilioni 465 ili zisaidie nchi kupata fedha za ruzuku kiasi cha Dola milioni 50.