Na
WyEST
kYRGYZSTAN
Wadau mbalimbali wa elimu Duniani wanakutana nchini Kyrgyzstan kujadili maendeleo na mageuzi ya elimu, ambapo imeelezwa kuwa walimu ni kitovu cha utekelezaji wa mageuzi hayo, elimu ya utunzaji mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yanafanyika katika mkutano ujulikanao kama School 2030 Global Forum unaoendelea kuanzia Juni 11 hadi tarehe 13 katika mji wa Bishkek nchini humo, ambapo ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo ambae ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba na wajumbe kutoka Aghakan Foundation na taasisi zingine za kijamii (CSOs).
Prof. Nombo ameshiriki akiwa mjumbe katika paneli ya kujadili namna ambavyo Tanzania inahakikisha kuwa walimu wanakuwa ni kitovu cha mabadiliko chanya katika elimu ikiwemo katika ufundishaji na ujifunzaji wa elimu ya mazingira ili kuhakikisha kuwa dunia na vizazi vijavyo vinakuwa salama na havipati athari ya uchafuzi wa mazingira.
Katika majadiliano hayo Prof. Nombo ameelezea mapitio makubwa ya Sera na Mitaala ya Elimu ya Ngazi ya Elimumsingi ambapo Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la Mwaka 2023 na mitaala iliyoboreshwa imeweka mkazo katika ufundishaji wa masuala ya utunzaji wa mazingira.
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania inafundisha masuala hayo kuanzaia elimu ya awali kama masomo yanayojitegemea na pia masuala ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabia nchi yamechopekwa katika masomo yote kwa ngazi zote za elimu.
Vilevile, amesema kuwa Tanzania inaendelea kutoa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini ili kuhakikisha kuwa walimu wanajengewa maarifa kuendana na wakati ikiwemo masuala ya mazingira. Prof Nombo pia alishiriki katika mjadala juu ya fursa zilizopo Tanzania ili kuanzisha ushirikiano na taasisi ya Global Education Solution Accelerator (GESA) inayojishughulisha na kutoa ufadhili kuwezesha kuharakisha utekelezaji mageuzi katika elimu.