Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali nchini wameendelea kutumia Elimu ya Watu Wazima katika nyanja mbalimbali ili kuisadia jamii kukabiliana na changamoto zilizopo.

Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo Oktoba 13, 2023 wakati akihitimisha Kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Juma la Elimu ya Watu Wazima lililofanyika Maili Moja, Kibaha Mkoani Pwani, ambapo ametumia fursa hiyo kupongeza jitihada hizo zinazoendelea kuwakomboa wananchi kuweza kupata elimu na  ujuzi.

Kwa kutambua umuhimu wa kuwa na taifa lililoelimika Mkenda ametaja program zinazotekelezwa, ikiwa ni Pamoja na Mpango wa Elimu Msingi kwa walioikosa (MEMKWA), Mpango wa Elimu kwa njia mbadala (AEP), Mpango wa Elimu Changamani kwa vijana walio nje ya shule (IPOSA),

‘’Nina amini katika mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo pamoja na Mitaala ambayo inafanyika tutaweza kuboresha program hizi ili kuongeza tija na kuwajengea uwezo vijana na watu wazima katika kuchangia uchumi endelevu na kuboresha maisha yao’’ alisema Prof. Mkenda.

Aidha Prof. Mkenda kwa namna ya pekee ameutambua mchango wa Shirika la Kimataifa DVV la nchini Ujerumani, pamoja na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kwa kuwezesha kuchangia kufanikisha Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima 2023.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, amesema Wizara imeandaa mfumo wa kutambua ujuzi  yaani _National Qualification Framework_ akiutaja kuwa ni mfumo wa kwanza kutumika hapa nchini, ambao umetambua program za Elimu ya Watu Wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.

‘’Kupitia Taasisi yetu ya Elimu ya Watu Wazima tumeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo, miradi ya elimu ya Sekondari nje ya Mfumo Rasmi ambapo kwa mwaka wa masomo 2023 wanafunzi wapatao 18,515 wameweza kudahiliwa. Elimu hii inatolewa kupitia Vituo vya Elimu Huria’’. Alisema Prof. Nombo

Ameongeza kuwa mkakati wa Kisomo unawezesha pia utekelezaji wa Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana walio nje ya Shule (IPOSA), ambapo jumla ya vijana 12,000 wamenufaika kupata mafunzo ya muda mrefu, wengine wamepata mafunzo ya muda mfupi hivyo kufanya jumla ya vijana 15,394 kuwa wamenufaika na mpango huu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Charles Msonde amesema kulingana mabadiliko yanayoikabili Dunia ni muhimu kutilia mkazo suala ya utolewaji wa elimu ya Watu wazima ili kuwezesha maarifa ya kutosha yanayohitajika katika Taifa hili.

Amesema kuwa "dhana ya elimu ya Watu wazima imezidi kuwa pana zaidi kadiri ulimwengu unavyobadilika, na sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI serikali imetupa majukumu makubwa ya kuhakikisha tunasimamia utekelezaji wa Sera yetu ya elimu ikiwa ni pamoja na elimu ya Msingi, Sekondari na elimu ya Watu Wazima" alibainisha Dkt. Msonde.

Kiongozi huyo ametoa rai kwa Viongozi wote pamoja na wadau kuendeleza utekelezaji wa mipango na program mbalimbali  za elimu ngazi zote, ikiwa ni pamoja na kushughulikia baadhi ya changamoto ili kuleta mapinduzi ya elimu katika taifa ikiwemo kuongeza umahiri katika lugha ya kiingereza.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Usimamiazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Dkt. Naomi Katunzi ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu chini ya mradi wa SEQUIP kwa kuipatia Taasisi hiyo jumla ya fedha TZS. Bilioni 5.6 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa madarasa na vituo vya elimu.

"Hii imewezesha kuwapa fursa mabinti waliopata ujauzito kurejea Shule na katika mazingira bora zaidi ya kujifunza, ni imani yangu kuwa tutaweza kutimiza ndoto zao" Alisema Daktari. Katunzi.

Pia amewashukuru wadau wa maendeleo UNICEF, UNESCO na Shirika la Kimataifa DVV kushiriki kikamilifu kufanikisha Maadhimisho hayo.

"Kwa muda huu UNICEF, kupitia Mradi wa Elimisha Mtoto wanafadhili utekelezaji wa Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA) unaotekelezwa kwenye mikoa ya Tabora, Kigoma na Songwe.