Uwezeshaji kupitia Ujuzi (ESP) ni mradi wa miaka 7 (2021-2028) unaotekelezwa na Jumuiya ya Vyuo na Taasisi za Ufundi Kanada (CICan) kwa ushirikiano wa karibu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Tanzania (MOEST) kupitia Idara ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (DTVET). Mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Kanada.
Lengo kuu la mradi ni Kuboresha Ushiriki wa Wanawake na Wasichana kwenye Shughuli za Kiuchumi nchini Tanzania. Mradi wa Uwezeshaji kupitia Ujuzi (ESP) utaimarisha njia mbadala za elimu, ajira, kujiajiri na ujasiriamali kwa wanawake na wasichana. Utafanya kazi na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) na Asasi za Kijamii (CBOs) katika Jamii 12 nchini Tanzania, Unalenga kuongeza viwango vya ushiriki kati ya wanawake na wasichana katika programu za mafunzo ya ujuzi na kuboresha upatikanaji wa mafunzo ya biashara, ujuzi, jinsia na haki za binadamu katika jamii zao. Mradi huu pia utapanua fursa katika sekta rasmi na zisizo rasmi kupitia usaidizi baada ya mafunzo ili kuingia kwenye ajira au kujiajiri.
Kupitia njia jumuishi na ushirikishwaji wa wadau muhimu, Wizara ya Elimu (MOEST), Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs), Asasi za Kijamii (CBOs), na kwa msaada wa viongozi muhimu wa jamii kushawishi mabadiliko ya kijamii, mradi huu utafanya kazi na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) 12 vilivyochaguliwa pamoja na Asasi za Kijamii (CBOs) 12 zilizochaguliwa kwa:
· Kuanzisha mtandao wa timu za jinsia na washauri wa kike;
· Kushirikisha jamii katika shughuli za kukuza uelewa wa kijinsia juu ya faida za elimu kwa wanawake na uwezeshaji wa kiuchumi;
· Kutoa mafunzo endelevu kwa washirika FDCs na CBOs ya kujenga uwezo katika usawa wa kijinsia, haki za binadamu, mbinu za ufundishaji na mafunzo ya watu wazima, uendelevu wa mazingira, CBET, uongozi, mwongozo na ushauri wa kazi, afya na usalama wa kazi (OHS), masoko / kuajiri, tehama (ICT), tathmini ya soko la ajira (LMA), uundaji na uwasilishaji wa programu zenye uhitaji.
· Kuendeleza na kutoa programu fupi za ujuzi wa kijinsia, mazingira na programu zenye uhitaji zinazolenga wanawake na wasichana katika vyuo washirika (FDCs);
· Kuendeleza na kutoa programu fupi za mafunzo ya ujuzi wa kijinsia na mazingira na mahitaji ya ujuzi katika Asasi za Kijamii (CBOs) ambazo ni washirika zinazolenga vikundi vya wanawake na jamii;
· Kupitia maudhui ya programu na mbinu za kufundishia ili kuleta muunganiko mzuri kati ya usawa wa kijinsia na haki za binadamu;
· Kusaidia Mpango wa Elimu Haina Mwisho (EHM) na programu ya Malezi na Makuzi ya Watoto na rasilimali za kujifunzia na kufundishia;
· Kuhakikisha kuna huduma sahihi za usaidizi kwa wanawake na mabinti, kina mama vijana katika vyuo (FDCs) washirika.
Malengo ya Programu kwa Asasi za Kijamii (CBOs) 12 zilizochaguliwa ni:
· Jumla ya wanawake na wasichana 480 watahitimu programu fupi za mafunzo ya ujuzi wa kijinsia zinazotolewa na Asasi hizi kwenye jamii.
· Jumla ya wafanyakazi wa kujitolea na wafanyakazi wakudumu 36 (24Ke) kutoka Asasi za Kijamii (CBOs) 12 watafundishwa juu ya ujuzi wa kiufundi na / au mbinu za ufundishaji na namna ya kutoa mafunzo ya usawa wa kijinsia na haki za binadamu.
· Jumla ya wanachama 2,400 (1,200Ke) watashiriki katika shughuli za usawa wa kijinsia na haki za binadamu.
Malengo ya Programu kwa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) 12 vilivyochaguliwa ni:
· Jumla ya wanawake na wasichana 720 watahitimu programu za muda mfupi za usikivu wa kijinsia zilizotengenezwa chini ya ESP.
· Jumla ya wafanyakazi 180 (60Ke) watapatiwa ujuzi wa kiufundi na / au mbinu za ufundishaji na namna ya kutoa mafunzo ya usawa wa kijinsia na haki za binadamu.
· Jumla ya wanafunzi 3,200 (1,000Ke) watashiriki katika shughuli za usawa wa kijinsia na haki za binadamu.