Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Calolyne Nombo na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweri wamekutana jijini Dodoma leo tarehe 11 Machi, 2024 kuweka mikakati ya pamoja ya mafunzo na utafiti katika kilimo.



Mazungumzo hayo yanakuja ikiwa katika hatua za utekekezaji wa Sera na Mtaala mpya wa Elimu hususani kwa upande wa Mkondo wa Elimu ya Amali ambao unajikita katika kujenga ujuzi, kilimo ikiwa sehemu ya mafunzo hayo.



Akizungumza katika kikao hicho Prof. Nombo amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwa na jukumu la kuandaa wataalamu, tafiti, kuchagiza ubunifu na kuimarisha matumizi ya Teknolojia, kupitia makubaliano hayo kutakuwa na ushirikiano katika kuendesha mafunzo kwa Vyuo vilivyo chini ya Wizara ya Kilimo pamoja na kuwezesha teknolojia mbalimbali zilizoibuliwa za kilimo kutumika.



"Kilimo ni moja ya Sekta kuu za kipaumbele hivyo kwa pamoja tunataka kuwa na mfumo mzuri wa kuzalisha wataalamu katika kilimo ambao watakuwa mahiri kulingana na mahitaji ya sekta hiyo na hivyo kuongeza tija katika mnyororo wa thamani wa sekta ya Kilimo na uzalishaji" amesema Prof. Nombo



Kwa upande wake katibu Mkuu Kilimo Gerald Mweri amesema Wizara hizo mbili zitashirikiana kutekeleza mradi Mkubwa unaojulikana kama from lab to Farm ambao utawezesha tafiti za kilimo matokeo yake kuwafikia wakulima kwa wakati.



"Tunajua kuna tafiti nyingi zimefanyika lakini haziwafikii wakulima, sasa kupitia mradi huu tunazitoa katika maabara, kwamba matokeo ya tafiti hizo tunayapeleka moja moja kwa mkulima", amesema Mweri.



Kupitia kikao hicho kamati maalum ya kuandaa mpango huo wa ushirikiano imeundwa na kutakiwa kuandaa na mpango mahsusi wa utekekezaji ndani ya muda mfupi.