Jumanne, 01 Septemba 2020 04:26

SEMAKAFU AVITAKA VYUO VYA FDC KUTOA PROGRAMU ZENYE UHITAJI KWA JAMII

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. AveMaria Semakafu amevitaka Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) kujikita katika kutoa mafunzo ya fani zinazopendwa na zinazotoa ajira badala ya kuendelea kuwa na fani ambazo hazina wanafunzi katika eneo husika.

Dkt. Semakafu ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua ukarabati na uendeshaji wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same kilichopo Mkoani Kilimanjaro ambapo amesema ni vizuri vyuo vikajiimarisha kwenye utoaji wa fani zenye wanafunzi wengi na kuachana na zile zenye wanafunzi wachache.

“Kuanzia mwaka huu, kila chuo cha wananchi kitafundisha fani ambazo zinahitajika katika maeneo husika kwa maana ya kuwa na wanafunzi wa kutosha hakuna chuo chochote kusajili fani ambazo zina wanafunzi wachache ama chini ya kumi na mbili, Serikali haiajiri walimu kufundisha wanafunzi wawili hakuna haja ya kuweka fani ambazo hazina wanafunzi wa kutosha” amesisitiza Dkt. Semakafu.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo amesema mpango wa elimu haina mwisho unaotolewa katika vyuo hivyo ni utaratibu wa kutoa fursa kwa watoto waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kijamii ili kuwasaidia kupata elimu na ujuzi wa kuwawezesha kuendelea na masomo na kuendesha maisha yao pindi watakapohitimu hivyo wanapaswa kufundishwa kama wanafunzi wengine bila kuwatenga.

Amesema serikali iliamua watoto hao wasome katika vyuo hivyo kupitia mfumo usio rasmi bila malipo yoyote kwa lengo la kuhakikisha wanapata fursa nyingine ya kuendelea na masomo na kuutaka uongozi wa chuo cha Maendeleo Same kuwawarudisha chuoni wanafunzi wote walioacha masomo kwa sababu mbalimbali ili waweze kumaliza masomo yao.

“Tumeanza program hii kwa lengo la kupata watoto wote walioacha shule na ndio maana unaona hata wasichana walioacha shule kutokana na changamoto mbalimbali tumewarudisha katika mfumo huu waje waendelee na masomo na na wale wenye watoto hata tuna shule za chekechea kwa ajili ya watoto wao” amesema Dkt. Semakafu.

Naibu Katibu Mkuu Dkt. Semakafu amekagua miundombinu iliyokarabatiwa na kuboreshwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo ameuagiza uongozi wa chuo hicho kufanya marekebisho katika baadhi ya miundombinu ambayo haikukarabatiwa vizuri.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya wananchi Same Edward Mdee ameishukuru wizara kwa ukarabati ambao umefanyika chuoni hapo, na kusema kuwa chuo hicho chenye wanafunzi 301 kipo katika mkakati wa kuboresha utoaji wa mafunzo ili kuhakikisha kinatoa vijana wenye ujuzi na maarifa yatakayowawezesha vijana wa Same kujiajiri ama kuajiriwa.

Read 430 times

Video News

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: 
  •               Mtaa wa Afya - Mtumba
  •               P.O.Box 10
  •               Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…