Alhamisi, 19 Desemba 2019 18:11

BILIONI 37 KUJENGA TAASISI YA TEKNOLOJIA DAR ES SALAAM (DIT) KAMPASI YA MWANZA

Serikali imezindua mradi wa ujenzi wa majengo mapya yenye thamani ya Sh. Bilioni 37 katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kampasi ya Mwanza kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia (World Bank).

Uzinduzi huo umefanywa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha alipomuwakilisha Waziri wa wizara hiyo kwenye mahafali ya kwanza ya Taasisi hiyo katika kampasi ya Mwanza ambapo amesema ujenzi huo utaanza karibuni na unatarajiwa kukamilika Desemba 2024.

Ole Nasha ameongeza kuwa mradi huo utaongeza udahili kwa zaidi ya asilimia 50 katika fani mbalimbali za ufundi na teknolojia na utawezesha kuhuisha mitaala katika fani ya ngozi ili kuzalisha mafundi mahiri watakaoweza kujiajiri na kuajiriwa.

Waziri Ole Nasha pia ametoa rai kwa wanafunzi waliopata mikopo kutumia fursa hiyo kusoma kwa bidii na kujiepusha na vurugu kwani zinaweza kuwaletea matatizo ikiwemo kuchukuliwa hatua na kukosa fursa za mikopo.

"Wanafunzi waliopata mikopo wajione kuwa wana bahati sababu kati ya wanafunzi zaidi ya elfu 70 wa mwaka wa kwanza walioomba ni 49,485 ndio waliopata, kwahiyo mnapopata fursa ya mkopo muitumie vizuri kwa kusoma na kujiongezea elimu kwa ajili ya maisha yenu ya baadaye," amesisitiza Ole Nasha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la DIT, Prof. Apollinaria Pereka akisoma historia ya DIT kampasi ya Mwanza amesema taasisi hiyo ilikidhi vigezo vya usajili wa kudumu kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) mwaka 2016 na kupewa kibali cha kuanzisha kozi ya teknolojia ya ngozi na sayansi na teknolojia ya maabara katika ngazi ya Stashahada.

Amesema anaamini DIT kampasi ya Mwanza itatekeleza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha inatoa wataalamu ambao wataifikisha nchi katika uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo mwaka 2025.

Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 11 wametunukiwa Stashahada ya sayansi na teknolojia ya maabara, wakiwemo wasichana wanne na wavulana saba.

Read 1248 times

Video News

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: 
  •               Mtaa wa Afya - Mtumba
  •               P.O.Box 10
  •               Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…