Jumapili, 21 Julai 2019 09:26

WAZIRI NDALICHAKO ATAKA USIMAMIZI THABITI UDAHILI WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ametoa wito kwa Viongozi wa Elimu ya juu nchini kuhakikisha wanasimamia ipasavyo mchakato wa udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2019/20 ili kuondoa usumbufu usiokuwa wa lazima kwa wanafunzi, wazazi, walezi na wafadhili wa wanafunzi hao. Waziri Ndalichako ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati akifunga maonesho ya 14 ya elimu ya juu yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi ambayo yalikuwa na kauli mbiu isemayo Jukumu la Taasisi za Elimu ya Juu Katika Kuzalisha Ujuzi Unaohitajika kwa ajili ya Viwanda. Katika hotuba yake amesema asingependa kuona changamoto zilizotokea mwaka jana katika kujiunga na vyuo zinajirudia kwani changamoto nyingine zilisababishwa na Vyuo vyenyewe kutokuwa na mifumo thabiti ambayo wanafunzi wangeweza kufanya maombi na kujithibitisha katika vyuo kwa urahisi. “Nafahamu kwamba TCU wameshatoa mafunzo na maelekezo ya kutosha kwa wataalamu wa mifumo ya kompyuta na maafisa udahili wa vyuo vyote ambao mnadahili wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2019/20 kwa hiyo naamini kwamba zoezi la udahili kwa mwaka huu litafanyika kwa ufanisi zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka jana,” alisema Waziri Ndalichako Waziri Ndalichako alisistiza kuwa kwa mujibu wa sheria ya vyuo vikuu sura ya 346 ya sheria za Tanzania jukumu la kudahili wanafunzi ni la Seneti za Vyuo Vikuu au Bodi ya za Chuo husika, hivyo amewataka Viongozi wa Vyuo kutumia mamlaka ya Seneti za Vyuo Vikuu au Bodi kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu udahili wa wanafunzi ili waweze kujiunga kwa urahisi huku akisistiza pia vigezo, masharti, taratibu na sifa za mwanafunzi kujiunga na chuo kuzingatiwa. “Niwakumbushe tu Serikali iko macho, katika mchakato wa udahili msipofuata taratibu mkaweka watu wasio kuwa na sifa tutawaondoa lakini kumbukeni na ninyi mloiwaingiza hamtabaki salama, hakikisheni zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi,”aliongeza Waziri Ndalichako. Sambamba na hilo amewataka wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo ya elimu ya juu kutokuwa wavivu wa kusoma maelekezo kabla ya kuanza kujiunga ama kuchagua kozi katika vyuo. Amewaasa kuzingatia sifa zinazohitajika kwa kulinganisha ufaulu wao wakati wa kuchagua kozi huku akisistiza kuwa Serikali haina utaratibu wa kumpangia mwanafunzi programu ya kusoma isipokuwa inachagua mwanafunzi kutokana na sifa alizonazo katika kozi husika. Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amezitaka Taasisi za Elimu ya juu na Vyuo vikuu kuendelea kujitathmini ni kwa kiasi gani tafiti ambazo wamekuwa wakizifanya zinagusa moja kwa moja jamii na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii. “Ninyi Taasisi za Elimu ya Juu macho yenu na masikio yawe wazi kila mara ili muweze kusikiliza wapi katiika jamii kuna changamoto na kwa kutumia utaalamu wenu mshiriki kuzitatua, kumbukeni elimu ya juu katika nchi yoyote ile ndio kitovu cha maarifa hivyo muendelee kutumika katika kutatua changamoto hizo,” aliongeza waziri Ndalichako. Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa maonesho Profesa Uswegi Minga Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Tumaini amesema uwepo wa maonesho hayo umetoa nafasi ya vyuo vyenyewe kujitangaza kuhusu fursa zinazopatikana katika vyuo vyao, lakini pia imekuwa nafasi nzuri ya kubadilishana uzoefu kutokana na kujifunza namna vyuo vingine vinavyofanya kazi hivyo kusaidia kufanya maboresho katika maeneo ya uendeshaji wa Vyuo lakini pia katika upangaji na ufundishaji wa programu mbalimbali. Maonesho hayo ya 14 ya Vyuo vya Elimu ya Juu yanaandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini na kwa mwaka huu yamekuwa na washiri zaidi ya 80 vikiwemo kutoka nje ya nchi na vile vyaTanzania. Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekenolojia. 20/07/2019
Read 1419 times

Video News

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: 
  •               Mtaa wa Afya - Mtumba
  •               P.O.Box 10
  •               Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…