Alhamisi, 11 Aprili 2019 08:00

WAZIRI MKUU MAJALIWA ASISITIZA UMUHIMU WA KUWA NA MITAALA INAYOKWENDA NA MABADILIKO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuona namna ya kuboresha mitaala ya chuo hicho ili kifikie viwango vya Elimu ya Juu.

Mhe. Majaliwa ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano la maadhimisho ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo amesema mpaka sasa chuo hicho kina majengo, sifa na kwamba elimu inayotolewa katika chuo hicho ndio inasisitizwa nchini.

Ameutaka uongozi wa chuo hicho kutia mkazo katika mafunzo ya uongozi hususan yale yenye mwelekeo wa kujenga uzalendo na kuendelea kutumia fursa ya kuwepo kwa makongamano kukuza uelewa wa jamii ya watanzania kuhusu umuhimu wa kuenzi falsafa za Mwalimu katika umoja, upendo, uzalendo, uadilifu na mshikamano wa kitaifa.

Aidha Mhe. Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwa kujenga misingi ya amani, umoja na kuleta maendeleo ya jamii nchini kwa vitendo na kuwataka watanzania kuzingatia maadili, uzalendo na utaifa katika uwajibikaji wa kila siku, kuungana kwa pamoja bila kujali itikadi za kisiasa au kikabila katika kulinda na kudumisha tunu hizo.

“Nimpongeze Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi anazochukua ili kuhakikisha anairejesha nchi yetu kwenye misingi yake ya awali ambayo ni kuwa na viongozi waadilifu, wazalendo na wenye kulinda amani na kudumisha umoja katika jamii, watanzania wote tunapaswa kuunga mkono jitihada hizi na kuzilinda kwa nguvu zote,” amesema Mhe. Majaliwa.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema ni vizuri kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuwa ni mtu ambaye amelipigania Taifa na kuliletea ukombozi na ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufuata nyayo za Baba wa Taifa.

Waziri Ndalichako ameeleza kufurahishwa na ushiriki wa wanafunzi katika kongamano hilo kwa kuwa linawapa fursa ya kupata uelewa mpana zaidi wa kile wanachofundishwa darasani, na kwamba taifa linawategemea kuwa chachu ya mabadiliko katika nchi.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji wa Chuo hicho, Steven Wassira alimweleza Waziri Mkuu kuwa wanaomba katika kumenzi Baba wa Taifa Chuo hicho kipandishwe hadhi na kuwa Chuo Kikuu na kwamba mazingira yake yaboreshwe yawe na hadhi ya Hayati Baba wa Taifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Prof. Shadrack Mwakalila amesema, Uongozi wa chuo hicho unaendelea na maboresho ya kutoa taaluma yenye kujenga uzalendo kwa vijana wa kitanzania.

Kongamano la Maadhimisho ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa limechagizwa na mada isemayo Mchango wa Mwalimu Nyerere katika kujenga Amani, Umoja na Kuleta Maendeleo ya Jamii nchini.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

11/04/2019

Read 1428 times

Video News

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: 
  •               Mtaa wa Afya - Mtumba
  •               P.O.Box 10
  •               Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
We use cookies to improve our website. By continuing to use this website, you are giving consent to cookies being used. More details…