Kongamano la Kimataifa la kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya Utalii na Ukarimu

Published on Tuesday 11 February, 2020 20:37:07

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amesema taasisi za mafunzo ya utalii na wadau wa sekta hiyo wanahitajika kufanya kazi kwa pamoja ili kutatua changamto zilizopo ikiwemo nguvu kazi yenye weledi na ufanisi wa kutosha katika tasnia hiyo.

Naibu Waziri Ole Nasha ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga Kongamano la Kimataifa la kuunganisha wanataaluma na wadau wa sekta ya Utalii na Ukarimu ambapo amesema ushindani katika soko ni mkubwa hivyo kunahitajika maandalizi mazuri ya rasilimali watu ili kuweza kushindana katika soko la dunia.

Amesema Utalii ni moja ya Sekta inayolipatia Taifa fedha za kigeni akitolea mfano mwaka jana 2019 nchi ilipata fedha za kigeni dola milioni 2.4 kutokana na utalii hivyo kukiwa na nguvu kazi yenye weledi na ufanisi wa kutosha nchi itaneemeka kupitia utalii.

“Hakika tunahitaji kuandaa vizuri rasilimali watu, nchi jirani zimepiga hatua kwenye kuvutia watalii sio kwamba wana vivutio vingi kuliko sisi ni kutokana na pamoja na mambo mengine kuwa na nguvu kazi yenye weledi ndio maana kama Taifa tunawekeza katika kutayarisha vijana ili kuwa na nguvu kazi yenye weledi katika sekta ya utalii," amesema Naibu Waziri Ole Nasha.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa kwa sasa utendaji kazi katika nchi yetu unalenga kuviimarisha viwanda ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuandaa nguvu kazi hivyo ni vizuri kukawa na mfumo wa mafunzo pacha kati ya Taasisi za mafunzo na wamiliki wa viwanda.

“Ninawiwa kusema kuwa kongamano hili limekuja kwa wakati muafaka sana na Wizara yangu itayachukua kwa uzito wake mapendekezo yote yaliyotolewa ukizingatia kuwa kuboresha muunganiko kati ya wanatasnia na wanataaluma ni moja ya vipaumbele katika wizara yangu ili kuhakikisha tunazalisha wahitimu bora watakaokidhi mahitaji ya soko la ajira,” aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha.

Naibu Waziri Ole Nasha amekipongeza chuo cha Taifa cha Utalii na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuandaa mkutano wa kuwaunganisha wakufunzi na waliopo kwenye biashara ya Utalii kwani kwa pamoja wanaweza kutatua changamoto zilizopo.

Naye Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Shogo Mlozi amesema kwa kushirikiana na vyuo vingine vinavyotoa mafunzo ya utalii wataendelea kuimarisha zoezi zima la utoaji mafunzo kwa kufanya kazi karibu na watoa huduma ili kupata nguvu kazi yenye weledi na ujuzi.

Kwa upande wake mshiriki wa kongamano hilo kutoka VETA makao makuu, Happiness Salema amesema ni vizuri kukawa na makongamano ya aina hii kwa kuwa yanawaleta pamoja watoa mafunzo na wamiliki wa viwanda, jambo ambalo linasaidia kuona changamoto zilizopo na kuweka mkakati kwani nchi zilizoendelea zinatumia mfumo huu katika kutoa mafunzo.

"Soko la hotelia na utalii liwe tayari kupokea mfumo wa mafunzo pacha hali kadhalika kuwa tayari kutoa nafasi kwa ajili ya walimu kupata ujuzi kwani kwa kufanya hivyo nchi itakuwa ya kwanza kuongoza kwenye sekta ya utalii na ukarimu," amesema Salema.

Kongamano la kimataifa la kuunganisha sekta ya Utalii na Ukarimu katika nchi zinazoendelea limefanyika kwa siku mbili Jijini Dar es Salaam na limewakutanisha wadau na wanataaluma katika sekta ya Utalii na Ukarimu kutoka nchi zinazoendelea.

Read 523 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top